| Chapter 10 |
1 | Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu, na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama moto.
|
2 | Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari, na wa kushoto juu ya nchi kavu,
|
3 | na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaaza sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo.
|
4 | Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni: "Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri; usiyaandike!"
|
5 | Kisha yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni,
|
6 | akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo. Akasema, "Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha!
|
7 | Lakini wakati ule malaika wa saba atakapotoa sauti yake, wakati atakapopiga tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama alivyowatangazia watumishi wake manabii."
|
8 | Kisha ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni pale awali ikasema nami tena: "Nenda ukakichukue kile kitabu kilichofunguliwa, kilicho mkononi mwa malaika asimamaye juu ya bahari na juu ya nchi kavu."
|
9 | Basi, nikamwendea huyo malaika, nikamwambia anipe hicho kitabu kidogo. Naye akaniambia, "Kichukue, ukile; kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali, lakini tumboni kitakuwa kichungu!"
|
10 | Basi, nikakichukua kitabu hicho kidogo kutoka mkononi mwa huyo malaika, nikakila; nacho kilikuwa kitamu kinywani mwangu kama asali, lakini nilipokimeza kikawa kichungu tumboni mwangu.
|
11 | Kisha nikaambiwa, "Inakubidi tena kutangaza ujumbe wa Mungu kuhusu watu wengi, mataifa, watu wa lugha nyingi na wafalme!"
|