| Chapter 11 |
1 | Mitume na ndugu kule Yudea walisikia kwamba watu wa mataifa mengine pia walikuwa wamelipokea neno la Mungu.
|
2 | Basi, Petro aliporudi Yerusalemu, wale Wayahudi waumini waliopendelea watu wa mataifa mengine watahiriwe, walimlaumu wakisema:
|
3 | "Wewe umekwenda kukaa na watu wasiotahiriwa na hata umekula pamoja nao!
|
4 | Hapo Petro akawaeleza kinaganaga juu ya yale yaliyotendeka tangu mwanzo:
|
5 | "Siku moja nikiwa nasali mjini Yopa, niliona maono; niliona kitu kama shuka kubwa likishushwa chini kutoka mbinguni likiwa limeshikwa pembe zake nne, likawekwa kando yangu.
|
6 | Nilichungulia ndani kwa makini nikaona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwituni, wanyama watambaao na ndege wa angani.
|
7 | Kisha nikasikia sauti ikiniambia: `Petro amka, chinja, ule.`
|
8 | Lakini mimi nikasema: `La, Bwana; maana chochote kilicho najisi au kichafu hakijapata kamwe kuingia kinywani mwangu.`
|
9 | Ile sauti ikasikika tena kutoka mbinguni: `Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa.`
|
10 | Jambo hilo lilifanyika mara tatu, na mwishowe vyote vilirudishwa juu mbinguni.
|
11 | Ghafla, watu watatu waliokuwa wametumwa kwangu kutoka Kaisarea waliwasili kwenye nyumba niliyokuwa nakaa.
|
12 | Roho aliniambia niende pamoja nao bila kusita. Hawa ndugu sita waliandamana nami pia kwenda Kaisarea na huko tuliingia nyumbani mwa Kornelio.
|
13 | Yeye alitueleza jinsi alivyokuwa amemwona malaika amesimama nyumbani mwake na kumwambia: `Mtume mtu Yopa akamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro.
|
14 | Yeye atakuambia maneno ambayo kwayo wewe na jamaa yako yote mtaokolewa.`
|
15 | Na nilipoanza tu kuongea, Roho Mtakatifu aliwashukia kama alivyotushukia sisi pale awali.
|
16 | Hapo nilikumbuka yale maneno Bwana aliyosema: `Yohane alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.`
|
17 | Basi, kama Mungu amewapa pia watu wa mataifa mengine zawadi ileile aliyotupa sisi tulipomwamini Bwana Yesu Kristo, je, mimi ni nani hata nijaribu kumpinga Mungu?"
|
18 | Waliposikia hayo, waliacha ubishi, wakamtukuza Mungu wakisema, "Mungu amewapa watu wa mataifa mengine nafasi ya kutubu na kuwa na uzima!"
|
19 | Kutokana na mateso yaliyotokea wakati Stefano alipouawa, waumini walitawanyika. Wengine walikwenda mpaka Foinike, Kupro na Antiokia wakihubiri ule ujumbe kwa Wayahudi tu.
|
20 | Lakini baadhi ya waumini waliotoka Kupro na Kurene, walikwenda Antiokia wakautangaza huo ujumbe kwa watu wa mataifa mengine wakiwahubiria ile Habari Njema juu ya Bwana Yesu.
|
21 | Bwana aliwasaidia na idadi kubwa ya watu iliamini na kumgeukia Bwana.
|
22 | Habari ya jambo hilo ikasikika kwa lile kanisa la Yerusalemu. Hivyo wakamtuma Barnaba aende Antiokia.
|
23 | Alipofika huko na kuona jinsi Mungu alivyowaneemesha wale watu, alifurahi na kuwahimiza wote wadumu katika uaminifu wao kwa Bwana.
|
24 | Barnaba alikuwa mtu mwema na mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana.
|
25 | Kisha, Barnaba alikwenda Tarso kumtafuta Saulo
|
26 | Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na lile kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko, kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo. ic
|
27 | Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu.
|
28 | Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote (Njaa hiyo ilitokea wakati Klaudio alipokuwa akitawala).
|
29 | Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea.
|
30 | Basi, wakafanya hivyo na kupeleka mchango wao kwa wazee wa kanisa kwa mikono ya Barnaba na Saulo.
|